Wednesday, April 3, 2013

NAULI ZAONGEZWA

WANANCHI wanaotaka kusafiri kwa mabasi ya mikoani, daladala katika Jiji la Dar es Salaam na wapandao treni ya Reli ya Kati, watalazimika kujikamua zaidi ili kupata huduma hiyo kuanzia wiki ijayo.
Hali hiyo inatokana na nauli za vyombo hivyo vya usafiri kupanda kwa baraka za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Viwango vipya vitaanza kutumika Aprili 12, ambapo nauli za daladala Dar es Salaam, zimeongezeka na kiwango cha chini kitakuwa Sh 400 huku cha juu kikiwa Sh 750.
Aidha, wanafunzi ambao hutakiwa kuonesha vitambulisho wanaposafiri, nauli imepanda kutoka Sh 150 hadi Sh 200 kwa safari ya umbali wowote ndani ya Jiji hilo. Uamuzi huo ulitangazwa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima.
Kwa mujibu wa Kilima, hatua ya kupandisha nauli hizo, imefikiwa baada ya kupitia mapendekezo ya wadau kuhusu kupanda kwa gharama za uendeshaji na kufanya michakato kujua uhalisia wake.
Daladala
Kutokana na uamuzi huo, kwa umbali wa kilometa kati ya sifuri na kumi, nauli itakuwa Sh 400 na mfano wa njia ya umbali huo ni Kivukoni- Ubungo.
Kwa umbali wa njia ya umbali wa kilometa 11 hadi 15, nauli itakuwa Sh 450 na mfano wa njia hiyo ni Mwenge-Temeke.
Kwa njia za kilometa 16 hadi 20, nauli itakuwa Sh 500 na mfano wa njia hiyo ni Tabata Chang’ombe - Kivukoni na kwa kilometa 21 hadi 25, nauli itakuwa Sh 600 na mfano ni kutoka Pugu Kajiungeni hadi Kariakoo.
Nauli ya juu kabisa Dar es Salaam, itakuwa Sh 750 kwa njia za umbali wa kilometa 26 hadi 30 na mfano wake ni njia ya Kibamba-Kariakoo.
Mikoani Akitangaza nauli mpya za mikoani, Kilima alisema nauli zitaongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, asilimia 16.9 kwa mabasi ya daraja la kati na asilimia 13.2 kwa mabasi ya daraja la juu.
Kutokana na hatua hiyo, kwa basi la kawaida kwa njia ya lami kwa kilometa moja, nauli itakuwa Sh 36.89 badala ya Sh 30.67 na kwa njia ya vumbi, nauli itakuwa Sh 46.11 kwa kilometa badala ya Sh 37.72.
Kwa basi la hadhi ya kati bila kujali lami au vumbi, nauli itakuwa Sh 53.22 kwa kilometa badala ya Sh.45.53. Kwa wanaopenda kusafiri na basi la hadhi ya juu pia bila kujali ni lami au vumbi, nauli itakuwa Sh 58.47, kwa kilometa badala ya Sh 51.64.
Ili kubaini daraja la basi husika na kulipa nauli kuendana na gharama, Kilima alisema wanaanza na mkoa wa Tanga ambapo mabasi yatawekwa vibao vya rangi kuonesha basi la daraja la juu litakalokuwa na rangi nyekundu, la kati bluu na la kawaida nyeupe.
Reli, tozo za bandari Kuhusu usafiri wa Reli ya Kati, Mamlaka hiyo ilieleza kuwa ongezeko la nauli kabla ya jipya, mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2009.
Alisema viwango vipya vya nauli za usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kwa daraja la kwanza ni Sh 75,700 badala ya Sh 60,599. Kutoka Dar es Salaam - Mwanza Sh 74,800 badala ya 59,818; Dar es Salaam-Tabora, Sh 54,800 badala ya Sh 43,859 na Dar es Salaam -Dodoma Sh 34,700 badala ya Sh 27,788.
Kilima alisema kwa daraja la pili, Dar es Salaam- Kigoma Sh 55,400 (44,305); Dar-Mwanza Sh 54,700 (43,747); Dar -Tabora Sh 40,500 (Sh 32,364) na Dar-Dodoma Sh 26,400 (Sh 21,092).
Kwa daraja la tatu; Dar –Kigoma Sh 27,500 (Sh 19,084), Dar-Mwanza Sh 27,200(Sh 18,860); Dar-Tabora Sh 20,400(Sh 14,173) na Dar-Dodoma Sh 13,500(Sh 9,374).
Kutokana na ongezeko hilo, Shirika la Reli Tanzania (TRL), limeelekezwa kutumia mfumo wa utunzaji taarifa za abiria, ambapo lilipewa mwaka mmoja kukamilisha uanzishwaji wa matumizi ya mfumo huo.
Pia ilitakiwa kuboresha mfumo wa kudhibiti mapato ya shirika, ili kuzuia uvujaji wa makusanyo ya fedha katika vituo ndani ya mabehewa, ambapo lilitakiwa kutekeleza kwa miezi mitatu.
Pamoja na kuboresha huduma ya usafirishaji abiria, pia lihakikishe lina mabehewa yenye huduma muhimu kama taa, maji safi, chakula na vyoo bora na safi na abiria wakikata tiketi na kupanda, waoneshe vitambulisho.
Akizungumzia ongezeko la tozo za kuhudumia meli katika bandari zinazomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kilima alisema TPA ilipendekeza kuongeza tozo kutoka asilimia saba hadi 400.
“Hata hivyo, Mamlaka imeridhia ongezeko la gharama kwa wastani wa asilimia 34.3, gharama ambazo kwa mara ya mwisho zilifanyiwa mapitio mwaka 1994,” alisema.
Alitaja tozo 19 zilizoongezwa kati ya huduma 100 zinazotolewa bandarini, kuwa ni tozo za nahodha kuingiza meli itakayokuwa dola 150, badala ya dola 122.05.
Tozo za bandari itakuwa dola 13.40, badala ya dola 10.00, tozo za kuongoza meli kuingia bandarini itakuwa dola 6 badala ya 4.50, tozo ya kuegesha meli, dola 0.50 badala ya 0.35.
Kilima alisema kabla ya kuanza kutoza viwango vipya, TPA inapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo iliyopewa, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa wateja.
Pia TPA ilitakiwa kuboresha usalama wa mizigo na shehena na kuimarisha ulinzi bandarini kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa.

CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment