Sunday, August 12, 2012

Mjue Anania Ngoliga



Alifikia kwa dada yake maeneo ya Msasani, kwa bahati nzuri sana jirani na alipofikia kukawa na jamaa aliyekuwa na gitaa, hivyo akawa analipiga mara kwa mara jambo ambalo likamfanya shemeji yake amuulize kwanini asijiunge na mojawapo ya bendi? Bahati nzuri huyo jamaa mwenye gitaa alikuwa anawafahamu baadhi ya wanamuziki wa bendi iliyojulikana kama Jambo Stars, iliyokuwa mali ya Dr Vulata, ikiwa na makao makuu Komakoma Mwananyamala. Hivyo Anania akaenda kuonana na wanamuziki wa bendi hiyo na kujitambulisha kama muimbaji, mwenyewe anasema alilazimika afiche kuwa anajua gitaa baada ya kusikia wapigaji wa magitaa waliokuweko katika bendi hiyo wakati ule, ambao walikuwa wazuri sana. Jambos aliwakuta Kazembe wa Kazembe, Cobra wa Bilumba ambao kweli walikuwa wapigaji wazuri wa magitaa, pia alimkuta Omari Gendaeka katika bezi na pia mpigaji mwingine Cheo Ali. Kwa hiyo baada ya majaribio akaonekana anafaa, hivyo akawa mmoja wa wanamuziki katika bendi ya Jambos. Aliendelea kupiga katika bendi hiyo mpaka siku moja ambapo mwanamuziki Lovy Longomba alipita kuangalia mazoezi yao, Lovy muda uleule akaamua kumchukua katika bendi yake ya Afriso Ngoma, hivyo basi akamwendea shemeji yake Anania na kumwomba amshawishi  Anania ajiunge na Afriso Ngoma, bendi iliyokuwa mali ya Mwendapole, na Lovy akiwa kiongozi wa bendi. 



          Kitime,  Anania
Anania mwenyewe anasema aliona kama ni ndoto, kwani si muda mrefu alikuwa katoka Mpwapwa na alikuwa hajawahi kupigia bendi yoyote, na kuja kuombwa na mwanamuziki kama Lovy kujiunga na bendi yake ilikuwa kama ndoto. Alienda kuripoti Afriso, bahati mbaya siku alipofika huko ilikuwa ndio siku Lovy anasafiri, kwa hiyo licha ya Lovy kuacha maagizo kwa wanamuziki wenzake kuwa wampokee Anania, na kwa uhakika zaidi wamfanyie interview. Hakuna mtu aliyeshughulika nae, Anania anasema anadhani jamaa walimdharau maana alikuwa bado hata viatu hajanunua alikuwa bado na viatu vya matairi alivyotoka navyo Mpwapwa na pia kwa kuwa alikuwa haoni, hawakumtilia maanani. Lovy aliporudi baada ya wiki mbili akakuta hata interview hajafanyiwa kwa hiyo akamuomba aimbe, nae akaimba vizuri nyimbo za Afriso, na kupata kazi mara moja, wakati waimbaji wa awali wawili Kasavubu na Anderson Supa wakapoteza kazi. Baadhi ya wanamuziki waliouweko wakati huo walikuwa John Maida, Robert Tumaini Mabrish, Mjusi Shemboza, Kasongo Kalembwe, Peter Kazadi wakiwa kwenye vyombo, Ramadhani Kinguti, Tofi Mvambe, Lovy na mwenyewe Anania kwenye uimbaji. Katika bendi hii walirekodi nyimbo nyingi ikiwemo Elly wangu na kusafiri  karibu wilaya zote nchini.
  Kutoka hapo akahamia Legho Stars wakati bendi inaanza kwa mara ya kwanza, waimbaji walikuwa yeye Anania, Shibanda Sonny, Marcelino Vitalis na Lucy Emea, kwenye vyombo Stamili Uvuruge, Chris Chiwaligo, George Mtully na Hemed Mganga. Baada ya Stamili Uvuruge na Shibanda Sonny kuondoka, ndipo akaja Tchimanga Assossa akiwa na na Jemsia Msuya, John Maeda na Shaaban Manyanya na kuanza awamu ya pili ya Legho Stars. Anania hakukaa sana akaiacha bendi hii kwa mara ya kwanza  na kujiunga na kundi la Ram Choc Stars liliyokuwa linaongozwa na Bi. Rukia Mtama, bendi hii iliikuwa na  waimbaji Banza Tax, Salim Shaaban, Adiel Makula, Chris Chiwaligo, Ado Mpoloto, Geofrey Charahani, kwenye rhythm Yahaya Mkango, bendi ilipata mkataba huko Iringa katika Iringa hotel, lakini wanamuziki wakawa hawalipwi kwa hiyo wanamuziki wakaondoka wote kwa pamoja siku ya mwaka mpya 1991….inaendelea

No comments:

Post a Comment