Tuesday, September 11, 2012

VIFO VYA ASKARI WA JWTZ SUDAN, BABA AZIMIA!

Mmoja kati ya familia ya Chacha akiwa anasaidiwa na wanajeshi baada ya kuzimia mara baada kuaga mwili wa marehem


KUFUATIA vifo vya askari watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokufa huko Sudan kufuatia gari walilopanda kusombwa na maji Agosti 25, mwaka huu wakati wakivuka mto vilisababisha mzazi mmoja wa wapiganaji hao kuzimia.
 Mzazi aliyezimia ni Matokeo Chacha Robogo ambaye ni baba mdogo  wa marehemu Julius Chacha.
Akizungumzia tukio hilo Robogo alisema kuwa alipatwa na mshituko mkubwa uliosababisha azimie mara baada ya kupokea taarifa ya kifo cha mwanaye huyo.
Mzazi huyo alikuwa na haya ya kueleza wakati alipohojiwa na waandishi wetu, eneo la Lugalo ambako miili ya askari hao ilifikishwa kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Nilikuwa nyumbani Tarime mkoani Mara  majira ya saa 4.30 usiku ndipo nilipigiwa simu na mtoto wangu aishiye jijini Dar es Salaam na kunitaarifu juu ya kifo cha Julius huko Sudan.
“Baada ya kupewa taarifa hiyo nilipata mshtuko nikaanguka chini na kupoteza fahamu, nilipozinduka nilijikuta nikiwa nimezungukwa na ndugu zangu.
“Nilipowauliza nilipatwa na nini wakanifahamisha kwamba nilipoteza fahamu baada ya kupewa taarifa za kifo cha Julius.
“Tulijisikia vibaya sana  kufuatia taarifa  hiyo kwani Julius alikuwa na mchango mkubwa sana katika familia yetu,  mwanangu huyo tulisoma wote katika Shule ya Msingi Kiongera, Tarime ambapo mwaka 1974 tulihitimu elimu ya msingi.
“Wakati tunasoma tulipatana sana na tulipohitimu masomo yetu tulijiunga na JWTZ  kwa lengo la kulinda nchi ambapo mimi muda wa kustaafu ulifikia kikomo mwaka 2001.
“Wakati akiwa Sudan alikaribia kumaliza muda wake ili arejee nchini, leo hii nashangaa tumepokea mwili,”  alisema baba mdogo huyo huku akibubujikwa na machozi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini, Jenerali Davis Mwamunyange alipohojiwa na gazeti hili katika viwanja hivyo vya Lugalo kuhusiana na vifo vya askari hao, alisema wamekufa kwa bahati mbaya.
 Tumepoteza nguvu kazi, kufa kwa askari watatu ni pigo kwa jeshi letu kwani hawakushambuliwa bali walikufa kwa kusombwa na maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.
Aliwataja askari waliopoteza maisha  kuwa  ni SSGT Julius Chacha, CPL Yusuph Chingwile na PTE Anthony Daniel na wote walisafirishwa kwenda kuzikwa makwao walikozaliwa.  

No comments:

Post a Comment