Ilikuwa ni saa kumi kasoro za jioni, jua la Dar es Salaam lilikuwa linawaka kama kawaida yake lakini halikuwazuia wakazi wa jiji hili maarufu kwa foleni za magari kuendelea na shughuli zao.
Wenye magari machafu yanayohitaji kuoshwa nao walielekea kwenye maeneo ya kuoshea magari ili kuyang’arisha.
Katika mitaa ya Mikocheni jirani kabisa na hospitali ya TMJ kwenye kituo cha mafuta cha Oil Com palikuwa kituo cha mwisho cha matembezi..
Tulipofika tulikaribishwa na mtu ambaye si mgeni katika macho yetu, Jaffarai. ‘Karibuni bana kwenye car wash yangu’ alituambia Jafarai kwa uchangamfu mkubwa.
Swali la kwanza kwa Jaffarai lilikuwa ni kuhusu umri wake leo katika siku yake ya kuzaliwa na kwanini ameamua kuzindua Car wash yake siku hii:
“Namshukuru mwenyezi Mungu nina miaka mingi ndio maana nafikiria sasa hivi kwakuwa umri umeenda nataka pia kipato kiende huwezi kuona umri unaenda halafu kipato kiko pale pale ndio maana nimeamua kufungua car wash kwasababu naangalia kitu tofauti kwasababu, nimefanya muziki kwa miaka kumi lakini nikaona kwamba nahitaji kitu kingine mbadala nje ya muziki kwasababu biashara ya muziki kama unavyoijua kuna sehemu unapanda kuna sehemu unashuka, kwahiyo nahitaji kuwa na biashara nyingine zaidi ya muziki ili kipush maisha yawe yanaenda,” anasema Jaffarai.
“Nilikuwa nizindue kama wiki mbili zilizopita nikasema acha nisubiri siku ya birthday yangu kwasababu hii inanipa motisha fulani sababu naona mwaka huu ambao ninauanza leo majukumu yanaongezeka hivyo inabidi niwe serious na vitu vingine nje ya muziki.
Plan ya kuanzisha car wash ni kwasababu nimeona ninataka kufanya biashara nyingine tofauti kidogo, sitaki kufanya biashara inayofanywa na watu wengine. Pia tuna uhaba wa car wash Dar es Salaam na magari yako mengi sana kama unavyojua, kila mtu ana gari siku hapa mjini unajua, car wash ziko chache halafu nyingi ziko local. Car wash ya kisasa kama hii hapa ni chache.”
Katika maongezi yetu anagusia pia mipango ya kuongeza matawi mengine ya car wash yake jijini kadri Mungu atakavyomjalia lakini anasema kuwa muziki bado ataendelea kufanya sababu ndio uliomfikisha hapo alipo.
“Muziki siwezi kuacha, muziki ndio maisha bila muziki hata hii car wash isingekuwepo. Kuna watu wazima mpaka leo wanaimba, kwahiyo nitaimba mpaka nitakapokufa.”
Jaffarai hakuacha kuwapa ushauri wasanii wengine wakongwe ambao maisha yamekuwa magumu na kubakia kulalamika kila siku. “Kubwa zaidi ni kujipanga kwasababu, tusijisahau sababu maisha ya ustaa ni maisha fulani ya kupita, hauwezi kuwa staa forever, tumeshasikia mastaa kibao walikuwa juu sasa hivi wameshuka. Kwahivyo wasanii wenzangu wajaribu tu kuinvest pembeni ya muziki yaani.
Haya maisha ni magumu kama wewe mwenyewe ukifanya yawe magumu lakini maisha sio magumu ukifanya yasiwe magumu. Watu wanatakiwa wajitume, unajua biashara ni kujaribu, Mungu mwenyewe anakuambia jaribu utapata, umejaribu mara ngapi? Hujajaribu hata mara moja unalalamika, jaribu kwanza ukishindwa kitu ndio uanze kulalamika kweli maisha magumu lakini jaribu kwanza.”
Car wash inaendelea kuchangamka na story zinanoga. Huu umekuwa mwanzo mzuri kwa Jafarai.
|
No comments:
Post a Comment