Tuesday, December 18, 2012

YALIOJIRI KATIKA KESI YA LULU...

MAKALI ya kesi ya mauaji inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael (Lulu) pichani, dhidi ya aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba, yamepunguzwa baada ya mshitakiwa kubadilishiwa mashitaka na sasa atasomewa ya mauaji bila kukusudia, mara jalada lake litakapofika Mahakama Kuu.

Awali, mshitakiwa alisomewa mashitaka ya mauaji na hadi kufikia jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjini Dar es Salaam, ilieleza wazi upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Taarifa hizo za kukamilika kwa upelelezi zilitolewa jana na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga, mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo.

“Mheshimiwa Hakimu, kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wa kesi umekamilika, mshitakiwa alitakiwa kusomewa muhtasari wa ushahidi, lakini Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, aliyekuwa na jalada hayupo.

“Mheshimiwa tunaomba tarehe nyingine ili mshitakiwa asomewe,” alisema Mtenga.

Wakili wa mshitakiwa, Peter Kibatala, aliiomba mahakama kupanga tarehe ya karibu ili mshitakiwa asomewe muhtasari wa ushahidi dhidi ya mashitaka yanayomkabili.

Hakimu Mmbando alikubali kuahirisha kesi hadi Desemba 21 mwaka huu, ili mshitakiwa asomewe muhtasari wa ushahidi na kisha jalada la kesi litafungwa, kesi itahamia Mahakama Kuu.

Hata hivyo habari za kuaminika zilizopatikana mahakamani zinasema, Lulu amebadilishiwa mashitaka hivyo baada ya jalada kufungwa, Mahakama Kuu itamsomea mashitaka ya kuua bila kukusudia.

Maofisa wa mahakama ambao walisema siyo siri, ni kweli mashitaka yalibadilishwa na pande zote zinazopingana zimepewa nakala ya mashitaka mapya.

“Hakuna siri tena, kila upande umepewa nakala ya mashitaka mapya, likishafungwa jalada atakwenda kusomewa Mahakama Kuu tuhuma za kuua bila kukusudia,” kilisema chanzo chetu.

Wakili Kibatala katika kuthibitisha hilo, alisema hata yeye amesikia taarifa hizo za mteja wake kubadilishiwa mashitaka ya awali ya mauaji, na sasa atashitakiwa kwa kuua bila kukusudia, lakini hakutaka kufafanua zaidi.

Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ni Kennedy Fungamtama, Kibatala na Fulgence Masawe.

Lulu yuko rumande kwa miezi nane sasa, kutokana na makosa ya mauaji kutokuwa na dhamana, anadaiwa kwamba Aprili 7 mwaka huu, maeneo ya Vatican, Sinza, alimuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.

ngasa we appreciated

No comments:

Post a Comment