Thursday, August 9, 2012

article thumbnailHukumu ya kihistoria leo

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo inatarajia kutoa hukumu ya Kesi ya Uhujumu Uchumi na Kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania, nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.
Profesa Mahalu na Martin wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Hukumu ya kesi hiyo iliyokuwa ikinguruma mahakamani hapo kwa miaka kadhaa sasa, inatarajiwa kusomwa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ambaye amekuwa akiisikiliza.

Awali, hukumu hiyo ilipangwa kusomwa Julai 11, mwaka huu lakini iliahirishwa kutokana na Hakimu Mugeta kukabiliwa na majukumu mengine. Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na kupanga kuwa hukumu hiyo itasomwa leo.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa washtakiwa hao, Mabere Marando alisema jana kwamba anaamini kesi hiyo ambayo imechukua muda mrefu, leo inafikia mwisho kwa Mahakama kutoa hukumu.

Hata hivyo, hakutaka kuizungumzia kwa undani hukumu ya leo badala yake alisema kuwa wanachosubiri ni kuona itakavyokuwa, ila wako tayari kwa matokeo yoyote.
“Sisi tunasubiri kuona hukumu ya Mahakama, kwani imekuwa ikisubiriwa sana. Kama akiachiwa tutafurahi na tutakunywa wine (mvinyo) usio na kilevi kama akifungwa basi tutapiga magoti kumwombea,” alisema Marando kwa utani huku akicheka.

Alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho ni wa Mahakama na kwamba mambo mengine yatafuata baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika makosa kama hayo yanayowakabili washtakiwa hao, ikiwa watapatikana na hatia adhabu yake inaweza kuwa kifungo kisichozidi miaka 15 jela.

Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Kifungu kidogo cha pili, Mahakama inaweza kutoa amri nyingine ikiwamo mshtakiwa kulipa fidia.

Hukumu ya kesi hiyo leo inasubiriwa kwa shauku si tu na Profesa Mahalu na wenzake ambao wangependa kujua hatima yao, bali pia na umma wote wa Watanzania ambao umekuwa ukiifuatilia kwa muda wote.

Wakati wa utetezi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake, alipanda kizimbani na kumtetea Profesa Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria.

Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa mchakato huo ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia alimmwagia sifa kedekede Profesa Mahalu akidai kuwa ni kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa umma.

Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.

Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwapo kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa aliifahamu mikataba yote hiyo na malipo kufanyika kupitia akaunti mbili tofauti.

Alieleza kushangazwa kwake kusikia kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, akisema hajui ni kwa nini Lumbanga alisema hivyo.

Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa waziri wake, Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Ujenzi na ile ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake. Alisema taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo ni sahihi.

Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi,” alisema Mkapa na kuongeza kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano.

Akijibu swali la Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa CAG kuhusu ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa hajawahi kupokea malalamiko hayo.

Akijibu swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia mikataba miwili, Mkapa alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa anahitaji ni kupata jengo.

Akijibu swali kwamba kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa kwa mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake, Mkapa alijibu: “Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Alhamdulillah.”

Pia Mkapa alisema anamshangaa wakili wa Serikali kudai kuwa pesa hizo kulipwa kwa awamu mbili kunaonyesha kwamba Profesa Mahalu alikuwa na lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake... “Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa (Mahalu) mimi namwamini.”

Utetezi wa Profesa Mahalu
Katika utetezi wake, Profesa Mahalu alikana mashtaka hayo na kudai kuwa alipofika katika ubalozi huo alikuta ofisi hizo zikiwa na hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake za mfukoni na kununua samani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi.

Alisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikwete pia alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya na kwamba aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.

Alisema mwanzoni mwa Juni, 2001 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge.

Alidai kuwa Katibu Mkuu alimtaka yeye na maofisa wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo. Alisema baada ya hapo aliwaagiza maofisa wake kwenda kutafuta majengo ndani na nje ya Jiji la Rome kwa ajili ya kulinunua.

Martin katika utetezi wake alidai kuwa, Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.

Akiongozwa na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Grace alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu mashtaka yote sita yanayomkabili hakuyatenda, aliwasilisha mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali.”

Pia Martin alihoji sababu ya upande wa Jamhuri kutomleta mmiliki wa jengo hilo la ubalozi kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo akidai walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi.

No comments:

Post a Comment