Thursday, August 9, 2012

Redondo arudi Simba, Sunzu aomba kuachwa





MWANDISHI WETU
MAZOEZI ya Simba yameanza rasmi jana Jumatatu huku ikimsajili kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo' wa Azam, lakini pia, Mzambia Felix Sunzu wa Simba ameomba kuachwa.

Redondo, ni mchezaji wa zamani wa Simba aliyekuwa akiichezea Azam FC, na sasa amerejea kwa mkataba wa miaka miwili.

Wakati hayo yakiendelea, Sunzu ambaye alisajiliwa na Simba akitokea klabu ya Al Hilal ya Sudan kwa mkataba wa miaka miwili, tayari ameitumikia msimu mmoja ambao Simba waliibuka mabingwa.

"Redondo amesajiliwa na Simba msimu ujao, Sunzu sijui kimempata kitu gani kwa sababu ameomba aachwe kwenye usajili wetu,"kilisema chanzo cha habari.

Hata hivyo Sunzu ameomba kwa mdomo kuachwa, lakini Simba imemtaka apeleke ombi hilo kwa maandishi.

Baadhi ya wadau wa klabu hiyo wanadai kuwa Mzambia huyo hana msaada na timu kwani alicheza chini ya kiwango katika michuano ya Kombe la Kagame, ambayo wapinzani wao Yanga ndiyo waliibuka mabingwa.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwanaspoti, Sunzu alisema: "Si kweli, siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa."

Sunzu alisajiliwa pamoja na Kago Gervais wa Afrika ya Kati ambaye alishindwa kung'ara na akatemwa mara moja.

Katika mazoezi ya Simba jana Jumatatu, wachezaji Haruna Moshi 'Boban', Mwinyi Kazimoto, Uhuru Suleiman na Juma Nyosso walimkosha kocha wao, Milovan Cirkovic,

ambaye alianza kwa mara ya kwanza kukifundisha kikosi hicho tangu arejee mapumzikoni Serbia.

Milovan ambaye alianza kazi rasmi ya kukinoa kikosi katika Uwanja wa Sigara, Chang'ombe alisema; "Nilikuwa na jaribio kwa wachezaji wangu na nilikuwa natafuta kasi.

Katika mazoezi hayo, Boban amefanya vizuri pamoja na Kazimoto, Uhuru na Nyosso pia kulingana na mazoezi niliyowapa,"alifafanua Milovan kwamba alitaka wakimbie bila mpira na kucheza na mpira kwa lengo la kuona uwezo wa kila mmoja.


No comments:

Post a Comment