EDO KUMWEMBE, LUBUMBASHI
KLABU yoyote ya Ulaya inayotaka kumnunua mshambuliaji wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta italazimika kuvunja benki na kutoa kitita cha Euro 10 milioni (Sh 19 bilioni), kwa mujibu wa mmiliki wa timu yake, Moise Katumbi.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini hapa, Samatta alisema Katumbi amemwambia kuwa timu yoyote inayomtaka barani Ulaya na kwingineko italazimika kutoa kitita kiasi hicho cha fedha ya kufuru kwa ajili ya kumnasa.
Samatta amekiri kwamba haoni kama ana thamani hiyo na badala yake kiasi hicho kitazifukuza timu nyingi ambazo zinamfukuzia kwa sasa.
�Katumbi ameniambia kuwa timu yoyote inayonitaka itabidi iweke ofa ya Euro 10 milioni mezani na mimi sidhani kama nimefikia thamani hiyo. Ni wazi itakuwa ngumu kwangu kuuzwa kwa sababu sioni mchezaji wa Afrika anayeweza kuuzwa kiasi hicho kwa sasa," alisema Samatta.
Mwanasoka wa Afrika aliyenunuliwa kwa bei zaidi ni Mghana Michael Essien, ambaye aliigharimu Chelsea kiasi cha pauni 24.4 milioni (Sh 58 bilioni) kutoka Olympic Lyon kwenda Chelsea mwaka 2005.
Hata hivyo , Samatta alikiri kwamba nia yake ya kwenda Ulaya ipo pale pale kama ilivyokuwa awali, lakini ana wasiwasi na nia ya Katumbi ya kuendelea kuwa naye.
"Bado nataka sana kucheza Ulaya. Nia yangu iko pale pale, lakini kama unavyomjua Katumbi ni mgumu katika kuuza wachezaji muhimu. Hata hivyo ipo siku nitamlilia niondoke," aliongeza Samatta.
Samatta alifunga bao jingine katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Jumamosi iliyopita wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Zamalek ya Misri.
Facebook comments for blogger brought to you by Eddie sucre?
No comments:
Post a Comment