Thursday, August 9, 2012

Vigogo wachuana uchaguzi UVCCM, UWT

ZAIDI ya wagombea 83 wamechukua na kurudisha fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi zilizotangazwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wakiwamo watoto na jamaa wa vigogo. Wakati mnyukano ndani ya UVCCM ukishika kasi, mpambano mkali unaonekana pia kuwapo katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), baada ya wagombea tisa wakiwamo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Terezya Huvisa na Mbunge wa Viti Maalumu, Rita Mlaki kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti.

Vigogo wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba ambaye ndiye mwenyekiti wa umoja huo sasa na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela. Mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ulikamilika jana.  UVCCM Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Oganaizesheni na Siasa UVCCM, Sophia Duma alisema makada hao 83 waliochukua na kurudisha fomu hizo, wanawania nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti na umakamu mwenyekiti.

 Wakati nafasi ya mwenyekiti ikiombwa na watu tisa, 18 wanawania nafasi ya makamu mwenyekiti. Makada hao wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Afrika Mashariki Paul Makonda ambaye pia ni mshirika wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma Anthony Mavunde na Mboni Mhita ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Kondoa Kaskazini. Wengine ni Mwenyekiti wa UVCCM, Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wengine ni Abubakar Asenga na Sango Gungu, Augustino Matefu, Ali Salum, Adolf Florian, John Beya, Peter Lwena na Innocent Melesi. Pia wamo Faidha Salum, Masoud Khamis, Felician Mtewele, Daud Mtungu na Theresia Mtelele. Nafasi nyingine ni 33 ambazo ni za kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC). Nafasi ya ujumbe wa Nec imeombwa na makada 33 uwakilishi wazazi wajumbe wanne na makada 32 wameomba nafasi ya Baraza Kuu ya UVCCM Taifa.

UWT Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makiladi alisema kwamba waliorejesha fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti wa umoja huo ni tisa na nafasi ya makamu mwenyekiti watatu. Aliwataja wanaowania nafasi ya mwenyekiti kuwa ni Sofia Simba, Anne Kilango Malecela, Maryrose Magige, Terezya Huvisa, Hamida Hassan Thabit, Halima Mamuya, Hilda Omary Kitana, Rita Mlaki na Raya John Safari.

“Waliorejesha fomu za kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Asha Bakari Makame, Asha Abdallah Juma na Sheilla Anna Ahmed,” alisema Makiladi. Alisema nafasi nyingine zinazowaniwa ni za wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Baraza Kuu UWT Taifa, Mwakilishi UWT kwenda mkutano wa UVCCM na Mwakilishi wa UWT katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi. Nafasi nyingine ni zile za kila mkoa ambazo ni Mwenyekiti, Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa, wajumbe wawili kutoka kila wilaya.

“Pia wapo ambao wanawakilisha wilaya zao katika baraza la mikoa na nafasi mojamoja kutoka jumuiya ya wazazi,” alisema  Makiladi. Alisema idadi ya wagombea wote waliochukua fomu itatolewa leo na kuongeza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, wamejitokeza wagombea wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment