Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, George Nyatogo.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
BODI
ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu nchini
(TCU) imewaengua zaidi ya wanafunzi 3074 walioomba vyuo na mikopo ya
elimu ya juu kwa mwaka 2012/13.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi hizo kupitia mitandao yao
(website) Agosti 10 na 12, 2012 zaidi ya wanafunzi 3074 wameenguliwa
katika maombi yao kwa kuwa na dosari mbalimbali.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) pekee
imeorodhesha zaidi ya wanafunzi 2,649 ambao imebaini kuwa na mapungufu
kadhaa katika maombi yao ya kupewa mikopo ya vyuo.
Miongoni
mwa makosa ama dosari ambazo bodi imezibaini kwa walioenguliwa kwa sasa
ni pamoja kukosekana kwa vyeti vya kuzaliwa kwa muombaji, sahihi ya
mdhamini/muombaji, kukosekana kwa picha ndogo ya muombaji/mdhamini,
kukosekana kwa sahihi za viongozi wa Serikali za mitaa/vijiji kwa
waombaji na nyaraka nyingine muhimu kwa waombaji.
Kwa upande wake TCU imewaengua jumla ya waombaji 425 kwa dosari na makosa mbalimbali, ambayo imeyabainisha katika taarifa yake.
Miongoni
mwa dosari ambazo zimetajwa na TCU kwa wanafunzi hao ni pamoja na
baadhi yao kukosea namba za vyeti vya masomo kwa vidato vya nne na tano
(O’ level na A’ level Index number), miaka ya kumaliza masomo (year of
completion), mawasiliano sahihi kwa muombaji (Contact information e.g.
Mobile phone number, email address and postal address) pamoja na
uchaguzi wa masomo (Programme selected).
Waweza kuingia katika linki hii hapo chini na kuona majina ya waliobainika kuwa na dosari anuai katika maombi yao kwa TCU http://www.tcu.go.tz
Pia
waweza kutembelea linki zifuatazo na kushuhudia majina ya waliobainika
kuwa na dosari hizo katika maombi yao kwa bodi ya mikopo;-http://www.heslb.go.tz
Hata
hivyo taasisi hizo mbili zimetoa muda kwa walioenguliwa sasa kutokana
na dosari hizo kurekebisha na kutuma tena maombi yao kupitia mitandao
kwa mujibu wa maelekezo waliyotoa.
Facebook comments for blogger brought to you by Eddie sucre?
No comments:
Post a Comment