Thursday, August 9, 2012

Yanga: Simba mmechokoza nyuki, subirini kilio, kisasi





MICHAEL MOMBURI
YANGA ipo jijini Kampala, Uganda na imetunisha misuli kwa kuapa kuwa italipiza kisasi kwa Simba na kujibu mapigo kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.

Alhamisi iliyopita, Rage alimnasa beki wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite ambaye pia alikuwa kwenye rada ya Yanga iliyokuwa imeshikiliwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na mmoja wa vigogo wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin Kleb.

Tangu Rage kushinda vita mjini Kigali, Bin Kleb hakuwahi kujibu na jana Jumatatu aliiambia Mwanaspoti kwamba amesikia mambo mengi yaliyosemwa na Simba na atajibu mapigo.

"Nilikuwa Kigali kwa mambo yangu ya kibiashara, lakini nashangaa Simba wamezungumza mambo mengi sana na kusema kwamba wamenigaragaza, sijapenda kujibu chochote, nilikuwa kimya tu. Sasa nimeingia Kampala kuna mambo ninafanya nimesikia wameendelea kujisifu tu."

Ingawa alidai kwamba hawakuwa wameelekeza nguvu kubwa kwa Twite, lakini habari za uhakika kutokana na jopo la usajili zinasema kitendo cha beki huyo kusaini Simba kimewapandisha hasira na watajibu na huenda wakakomoa zaidi na kuonyesha jeuri ya fedha na kiburi cha uongozi mpya.

"Wanasema mimi ni bwana mdogo siwawezi kwa fitna na ujuzi wa mambo ya mpira, wanasema sina uzoefu wowote kwenye mambo ya mpira, sasa ninachosema ni kwamba huyo Rage nimemsoma na lazima nilipize kisasi, siwezi kuvumilia maneno yao.

Wanaongea sana mpaka vitu vingine ambavyo havipo kabisa,"alisisitiza Bin Kleb na kudai kuwa yupo Kampala na uwepo wake huko utatambulika na utawaadhiri Simba wanaomponda.

"Sisemi ninafanya nini Kampala lakini naahidi kishindo changu kitasikika,"alisema kiongozi huyo ingawa alipoulizwa kama ndio wanakamilisha mipango ya kuvunja mkataba wa Emmanuel Okwi na Simba akacheka na kuahidi ndani ya muda mfupi kishindo kitasikika.

Mwanaspoti linajua kwamba Yanga inamshawishi Okwi kuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliosalia kati yake na Simba, baada ya kubainika kuwa uwezekano wa kwenda kucheza Austria kwenye klabu ya Redbull Salzburg umefutika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni ni kosa kuzungumza na mchezaji mwenye mkataba wa zaidi ya miezi sita na klabu yake.

Lakini habari za ndani zinadai Yanga mpaka leo Jumanne jioni itakuwa imeshajua mbivu na mbichi na kama ikishindikana itasaini straika mwingine kinda wa timu ya taifa ya Uganda pamoja na beki mmoja wa kati wa timu moja ya Ligi Kuu Bara.

Simba imetangaza kuwa Okwi atatua leo Jumanne kuungana na wenzake kwa ajili ya Simba Day kesho Jumatano.

Kwenye usajili wa Yanga hadi sasa kuna wachezaji wanne wa kigeni ambao ni Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza wa Uganda, Mrundi Didier Kavumbagu na Yaw Berko wa Ghana.

Usajili wa kwanza wa Ligi Kuu Bara unafungwa Ijumaa ijayo na siku nane zinazofuata baada ya hapo itakuwa kuhakiki majina na kukamilisha uhamisho.

Simba imetangaza kuwa klabu yoyote inayomuhitaji Okwi itatakiwa kulipa Shilingi bilioni moja.


No comments:

Post a Comment