OLIVER ALBERT
KOCHA wa Simba Milovan Circovic amemzungumzia Mrisho Ngassa huku akisema ana siku 15 za kukisuka kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Septemba Mosi.
Milovan amekiri hakuridhishwa na kiwango cha timu yake kwenye michuano ya Kagame na anataka akisuke tena ili akirudishe hadhi yake kama ilivyokuwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
"Hatukucheza vizuri Kagame nafikiri kutokana na ugeni wa baadhi ya wachezaji, kuanzia Jumatatu (jana) nina siku 15 tu za kuhakikisha wachezaji wangu wanakuwa fiti na tayari kwa mapambano kwenye Ligi Kuu,"alisema.
"Tumeshindwa kuchukua Kagame hivyo hatutaki kukubali tufanye vibaya kwenye ligi na kukosa ubingwa, timu yangu ni nzuri ila kuna kasoro ndogo ndogo ambazo ndani ya siku hizo nitakuwa nimezirekebisha na timu itarudi katika hadhi yake, mashabiki wasiwe na wasiwasi kwani mambo mazuri yanakuja na kila mmoja atakubali ninachokizungumza," alisema Milovan.
Kuhusu Ngassa alisema; "Kama unavyojua kikosi changu kilikuwa na upungufu mkubwa katika sehemu ya ulinzi hasa beki ya kati na ushambuliaji lakini kusajiliwa kwa watu hao wawili kumeleta matumaini mapya katika klabu yetu.
"Ngassa ni mchezaji mzuri sana, ana kasi, mjanja na anafunga mabao na ni mmoja ya wachezaji waliokuwa chaguo langu kwenye usajili kwa ajili ya msimu ujao pia hata Twite(Mbuyu) ni beki makini sana , nimemuona Kagame nafikiri ni beki bora wa mashindano yale hivyo atasaidia sana," alisema Milovan.
Simba ina tatizo kubwa la beki ya kati kutokana na kuondokewa na beki wake tegemeo Kelvin Yondani ambaye amehamia Yanga.
Facebook comments for blogger brought to you by Eddie sucre?
No comments:
Post a Comment