Taarifa ya kukamatwa kwa askari hao imekuja siku moja baada ya kubainika kwamba, askari kadhaa walioendesha operesheni dhidi ya wafuasi wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha Mwangosi walitoka mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro.
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na baadhi ya askari polisi mkoani Iringa na Makao makuu jijini Dares Salaam, zilisema kuwa polisi hao, akiwamo yule aliyeonekana kwenye picha za video na za mnato akimlipua kwa mtarimbo wa bomu la machozi (jina tunalo) wamekamatwa na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Iringa.
Kwa mujibu wa habari hizo, askari hao walikamatwa Jumatatu wiki hii ikiwa ni siku moja baada ya mauaji hayo yanayoaminika kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kutumia askari wa mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani.
"Hivi sasa (jana mnamo saa 8:30 mchana) ninapozungumza na wewe bado hao askari wanaendelea kuhojiwa. Wako watano," alisema askari polisi mmoja aliyekuwa karibu na chumba wanachoshikiliwa askari hao.
Chanzo hicho kilieleza kuwa askari aliyemuua Mwangosi alionyesha kusikitikia tukio hilo akisema hakukusudia kufanya hivyo.
"Anasema ni kwamba, yeye mwenyewe hakupenda kuona tukio hilo likitokea. Aliniambia kuwa kifo cha mwandishi huyo kimemsikitisha sana, na nilipomuuliza nini hasa kilitokea, alisema; ahh hilo niache nitaeleza nitakapohojiwa," kiliongeza chanzo kilichokuwa karibu na askari huyo.
Afisa Upelelezi wa Ukoa wa Iringa, (RCO), SSP Nyigesa Wankyo hakuthibitisha kuwashikilia askari hao, badala yake akataka kazi hiyo ifanywe na polisi Makao Makuu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na simu yake ya mkononi haikuwa inapatikana hadi tunaenda mitamboni.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kamishna Robert Manumba alisema; "Wakati ukifika mtaambiwa. Kwa sasa muda haujafika, subirini uchunguzi uendelee, mtaambiwa".
Polisi aliyelipuliwa mguu anena
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya askari waliokuwapo wakati tukio zima lililosababisha kifo cha Mwangosi ambaye alijeruhiwa katika mguu wake wa kushoto na kupoteza fahamu kabla hajafikishwa hospitali ya wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa anaendelea vizuri na matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo, Aseri Mwampamba alisema alipoteza fahamu baada ya kujeruhiwa katika mguu wake wa kushoto.
"Ni kweli nilikuwa eneo la tukio baada ya kuona hali ya amani katika eneo hilo imekuwa si nzuri, wanachama hawakutaka kuondoka eneo la mkutano. Wakaanza kufanya vurugu na kusababisha nikajeruhiwa mguuni kama unavyoona," alisema Mwambapa.
Alipotakiwa kueleza majeraha hayo aliyapataje, askari huyo alisema hata yeye hafahamu isipokuwa akiwa amesimama alishangaa kuona kitu kikitua mguuni na kwamba anadhani kilitoka chini na kutua katika mguu wake wa kushoto.
Hata hivyo, picha za mnato zilizochapishwa kwenye magazeti mbalimbali nchini baada ya tukio hilo, zimeonyesha kuwa mara ya mwisho Mwampamba alionekana amekumbatiwa na marehemu Mwangosi huku askari mmoja alilenga mtarimbo wa kufyatua mabomu ya machozi.
Jaji Ihema aja juu
Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi, Jaji Mstaafu Stephen Ihema amesema katika historia yake ya utumishi wa umma hajawahi kushindwa kazi.
Alisema amesikitishwa na kauli za kubeza uteuzi wake zilizotolewa na viongozi wa Chadema, waliopinga uteuzi wake.
Huku akitumia kitabu cha Bibilia kutetea utendaji wake, Jaji Ihema alisema amesikitishwa na matamshi hayo ambayo yanavunja moyo na hayakupaswa kutolewa.
“Haya ni maoni tu ya mtu ambayo yanaweza kuwa sahihi kwa mtoaji na yakawa siyo sahihi kwa upande wa mwingine.
“Pili, napenda niseme kwamba hayo maoni is not biblical conclusive(msaafu ambao hautiliwi shaka)” alisema Jaji Ihema alipoulizwa na gazeti hili jana.
Pamoja na kukataa kujibu tuhuma hizo, Jaji Ihema alisisitiza kwamba, anafahamu vema siasa za nchi hii na kuwataka wanaohoji utendaji wake wafuatilie rekodi yake ya nyuma.
Wakati akiwasilisha msimamo wa Chadema kupinga uteuzi wa jaji huyo kuongoza kamati hiyo, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu alidai kuwa kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Ihema hana uwezo na kazi ya ujaji na mpaka sasa alikuwa ana kesi 300 ambazo anashindwa kuzitolea uamuzi.
Lakini, Jaji Ihema amepuza tuhuma hizo akisema; “Haya ni matamshi ya kisiasa tu, na mimi nazijua siasa za Tanzania”.
Aliongeza; “Ninachoweza kusema mimi ni kwamba, nimeteuliwa kuwa kiongozi wa kamati hii, na ukiniuliza mimi nimepokeaje nitakuambia, this is not any issue (yaani siyo jambo la kujadiliwa sasa). Kama unataka kujua vigezo vipi vilivyotumika nitakuambia nenda kwa Waziri nadhani yeye anajua, alipokea ushari wa watu gani na baadaye akafikia uteuzi huo.”
Katibu WAPC aonya
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC), Christopher Conybeare, amelaani mauaji ya mwanahabari Mwangosi, yanayodaiwa kufanywa na polisi na kuagiza hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika wa tukio hilo.
Conybeare alisema hayo jana katika hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania(MCT), kwa ajili ya WAPC na kusisitiza kuwa uchunguzi wa tukio hilo hauna budi kufanyika haraka iwezekanavyo ili hatua zichukuliwe mapema kutokana na unyeti wa sekta ya habari duniani.
Katibu huyo ambaye yupo nchini kwa ajili ya mkutano mkuu wa WAPC pamoja na wajumbe 15 kutoka mabaraza mbalimbali ya habari duniani, alisema tukio hilo linaweza kuiharibia sifa Tanzania kwani ni moja ya nchi zenye taswira nzuri duniani katika tasnia ya habari na kuongeza kuwa wanahabari wanapouwawa, demokrasia nayo hufa.
“Mauaji ya mwandishi nimeyasikia kwa sababu nipo hapa nchini tangu Agosti 29, na ni jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa haraka kwani linaharibu maana ya demokrasia,” alisema Conybeare.
Conybeare aliimwagia sifa MCT na kusema kuwa ni miongoni mwa mabaraza makini duniani ambalo watanzania wanatakiwa wajisifie kwa kuwa nalo.
“Nimeifahamu MCT mwaka 2003 katika moja ya mikutano ya WAPC, na tangu wakati huo tumekuwa tukifanya kazi pamoja na nimefurahi sana mkutano huu kufanyika Tanzania.” Alisema
Jukwaa la Katiba
Nalo Jukwaa la Katiba Tanzania limesema Kamati ya watu watano iliyoundwa na waziri Nchimbi kuchunguza kifo cha Mwangosi ni batili.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa jukwaa hilo Deus Kibamba alisema; “Kwa kuwa uchunguzi unaofanywa hauhusiani na kilichomuua Mwangosi wala kundi gani limemuua, tunataka Kamanda wa Iringa asimamishwe kazi kupisha uchunguzi, tume iundwe na rais na kusimamiwa na mahakama.”
Alisema kuwa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo ipelekwe bungeni na rais Kikwete ili wabunge wapate fursa ya kuijadili na kutoa maamuzi ya kibunge.
“Kamati ya Nchimbi ni batili kwa sababu mtu au kundi hawezi kuwa hakimu wa kesi inayomhusu mwenyewe, isipofanyika hivyo, tume hiyo haiwezi kufanya kazi yake kwa uhuru” alisema Kibamba na kuongeza:
“Athari za matukio ya mauaji na fujo zinazosababishwa na jeshi la polisi kutawanya waandamanaji au mikusanyiko ya watu kutaathiri hata mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya, kwa kuwa watu wataogopa kujitokeza”
Bavicha Iringa
Wakati huo huo, siku moja baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kutishia kukifuta Chadema kutokana na matukio ya vurugu katika mikutano yake, Katibu mkuu wa Baraza Vijana Tanzania (Bavicha), Deogratias Munishi amesema kabla ya kuifuta Chadema ni vyema akaanza kukifuta Chama Cha Mapinduzi(CCM), kwa madai Serikali yake ndiyo chanzo.
Munishi alitoa kauli hiyo, akijibu kauli ya Tendwa akisisitiza kuwa, ushahidi wa tukio lililotokea Nyololo, Mkoani Iringa juu ya nani aliyeanzisha vurugu na namna mauaji hayo yalivyotokea wanao na kwamba, wapo tayari kuutoa wakati wowote kwa kamati huru na ya kuheshimika.
“Kama Tendwa anataka kuifuta Chadema, basi aanze na CCM kwa sababu tunamjua anatumwa na CCM kukiharibu chama chetu wakati Serikali yake kupitia Jeshi la Polisi ndiyo yenye vurugu, na imekuwa ikisababisha mauaji mengi ambayo, hakuna asiyeyajua,” alisema.
Alisema jeshi hilo halina namna yoyote ya kukwepa, mauaji ya Mwangosi na kulitaka kuacha kutoa kauli za kuwasingizia wananchi kwamba, kuna mmoja wao alirusha bomu kuelekea kwa mwandishi huo, wakati wapo waliokuwa wakishuhudia na wengine walichukua picha za tukio zima, wakiwemo waandishi wa habari wenyewe.
“Polisi ndio ambao wamekuwa wakiua raia, ukiangalia picha zilizopigwa eneo la tukio hakuna mtu asiyeona jinsi polisi walivyomuadhibu Mwangosi kabla ya kumuua,” alisema Minishi
Chanzo Mwananchi
Facebook comments for blogger brought to you by Eddie sucre?
No comments:
Post a Comment