Elizabeth Edward
UBUNIFU unaweza kuwa nyezo muhimu katika kuhakikisha sanaa inachangia kulinda maadili ya Kitanzania, ambayo hata hivyo kadri siku zinavyokwenda, yanaonekana kupotoshwa kwa kuiga tamaduni za watu wengine.
Hivyo, sanaa ikitumika vyema, inaweza kuwa nguzo katika kukuza na kulinda maadili bora ya Kitanzania.
Hili litawezekana iwapo sanaa itazingatia mila na desturi zetu na kuacha kuiga tamaduni za watu wengine.
Huo ni mtazamo wa msanii maarufu wa vichekesho, Hemed Maliyaga maarufu Mkwere.
Muigizaji huyu anayefanya vizuri kwenye sanaa ya vichekesho kupitia kundi la Mizengwe.
Mkwere anafahamika zaidi kutokana na vituko vyake, ambavyo licha ya kuwepo kwa wasanii wengi wa vichekesho nchini, anabaki kuwa msanii mwenye mvuto wa aina yake.
“Watu wanadhani kuiga mambo ya kizungu ndiyo ujanja, hawaelewi kuwa hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili na kuacha tamaduni zetu, zinazolinda utu wetu kama Watanzania,”anasema Mkwere.
Anaongeza kuwa Watanzania sasa wamekuwa na mwamko mkubwa katika sanaa hivyo ni jukumu la wasanii kuhakikisha kazi zao zinazingatia, maadili ili kuifanya jamii nzima kuwa huru kuangalia, bila kuhofu maudhui yaliyomo.
“Kwa sasa kuna kazi za sanaa zinazoingaliwa kwa rika, hiyo inatokana na mambo ya ajabu yanayooneshwa humo. Hii inasababishwa na kukosa ubunifu,” anasema.
Hata hivyo, Mkwere anatahadharisha kuwa wasanii wengi nchini hawana vipaji vya usanii, hivyo kuishia kulazimisha kufanya mambo waonekane ni wasanii wakati hawana uwezo.
Anasema kuwa sanaa inapaswa kuwa chachu ya maadili mema na chanzo cha ajira kwa vijana ikiwa watatumia akili zao kubuni mambo yanayoweza kuuzika katika soko.
“Vijana watambue kuwa sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira. Naweza kumudu mahitaji ya familia yangu kutokana na sanaa, hiyo inatokana na ubora wa kazi ninayoifanya,” anasema Mkwere.
Kuhusu familia
Mkwere kwa sasa ni baba wa mtoto mmoja. Anasema kuwa anapata faraja kwa kuwa familia yake inamuunga mkono kwa kiasi kikubwa kwa kazi anayofanya ingawa, ipo katika mazingira magumu.
Anafafanua kuwa watu wengi wanachukulia kazi yake kama ni kituko, lakini mke wake amekuwa mwelewa na mwenye kumtia ili aendelee kufanya kazi hiyo.
“Nashukuru mke wangu ni mwanamke mwelewa, amekuwa msaada mkubwa kwangu, namtegemea kwa ushauri na mawazo. Kwa kweli navijunia kuwa na mwanamke wa aina hii, kwani anaelewa vizuri kazi yangu ingawa watu wanaona nafanya vituko, lakini yeye anajua nipo kazini,”anasema.
Anaongeza kuwa mara nyingi hutumia muda wake wa mapumziko kukaa na familia yake, ambapo hupata fursa ya kumsaidia mkewe kazi mbalimbali za nyumbani sambamba na kujadili masuala yanayolenga kujenga familia .
“Muda ninaopata nafasi ya kuwa na familia yangu napendelea kuweka vikao, kujadili mambo mbalimbali kwa kuwa mara nyingi nakuwa na shughuli za kikazi ambazo huchukua muda wangu mwingi,” anasema.
Nje ya sanaa Mkwere ni mshereheshaji katika shughuli mbalimbali pamoja,pia ni mjasiriamali wa biashara ndogondogo zinazochangia kuongeza kipato cha familia yake.
Kuanza sanaa
Mkwere alianza kujihusisha na sanaa mwaka 1994 akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na alipita katika vikundi mbalimbali vya sanaa.
Alianza kujulikana alipojiunga na Kikundi cha Sanaa cha Mizengwe kuziba nafasi ya marehemu Max.
Mkwere anasema yeye hakuwa na undugu na marehemu Max na kuongeza kuwa alimfahamu kupitia sanaa.
“Huenda watu wanatufananisha sura, lakini sikuwa na undugu naye kabisa ingawa tumetoka mkoa mmoja na kabila letu ni moja,” anafafanua.
Mkwere anasema anakerwa sana na tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa Watanzania.
Anaeleza kuwa kwa sababu hiyo vijana wengi wamejikuta wakishia vijiweni na kufanya mambo yasiyo ya msingi.
“Ningepata nafasi ya kuwa kiongozi katika nchi hii jambo la kwanza kulishughulikia ni tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa Watanzania. Utakuta watu wanatumia siku nzima kupiga zogo badala ya kufanya shughuli mbalimbali za kuingiza kipato,”anasema Mkwere.
EDITED BY EK 01/08/2012
Facebook comments for blogger brought to you by Eddie sucre?
No comments:
Post a Comment