Thursday, August 9, 2012

PAPAA MSOFE AFIKISWA KWA IGP MWEMA

Papaa Msofe.
Na Makongoro Oging’
MARY Kituli (40), mkazi wa Jiji la Dar es Salaam amedai kuwa maisha yake yapo hatarini tangu marehemu mumewe, Chasphori Kituli auawe kwa kupigwa risasi nyumbani kwake, Magomeni Mapipa wilayani Kinondoni, hivyo kuamua kulifikisha sakata hilo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema.
Mjane huyo ameliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa amemuomba IGP Mwema kumpa ulinzi kutokana na hofu hiyo kwa kuwa amekuwa akipata vitisho kama alivyovipata mumewe kabla ya kuuawa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela, polisi wanamshikilia Marijani Abubakari maarufu kwa jina la Papaa Msofe kutokana na mauaji hayo.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa mafichoni na mwandishi wa habari hii, Mary ameeleza kwamba vitisho vimekuwa vingi, jambo ambalo linampa hofu kubwa na kuamua kujificha.
Mary aliendelea kusimulia mkasa mzima kuhusiana na misukosuko iliyowapata kuanzia mumewe alipouawa hadi sasa kama ifuatavyo:
“Marehemu mume wangu alikuwa mfanyabiashara na alikuwa akimiliki migodi Mererani, Arusha. Tulikuwa tunaishi Mikocheni A na watoto wetu wawili.
“Nakumbuka mgogoro uliokuwepo ni baina ya mume wangu na mfanyabiashara mmoja maarufu nchini (jina linahifadhiwa) ambaye alidai kwamba amempa marehemu Sh. milioni 30, akasema akishindwa kurudisha atachukua nyumba yetu iliyopo Mikocheni.
“Tukasikia kuwa nyumba yetu hiyo baadaye alimuuzia Papa Msofe lakini sisi hatukuweza kuhama kwa kuwa makubaliano hayakuwa hivyo.
“Oktoba 2007 tulivamiwa nyumbani hapo na watu tunaowafahamu, wakachukua vitu mbalimbali likiwemo gari aina ya Range Rover pamoja na bunduki aina ya shotgun. Vitu hivyo hatujavipata hadi leo.
“Kufuatia kitendo hicho tuliamua kuhamia Magomeni Mapipa huku tukiendelea na kesi ambayo mume wangu aliifungua baada ya kutokea kwa tukio hilo. “Ilipofika Oktoba 3, mwaka jana mume wangu aliendelea kupata vitisho, wanafamilia tukaingiwa na woga.
“Ilipofika Oktoba 6, 2011, mume wangu akiwa ndani ya gari kwenye geti la nyumba yetu ya Magomeni Mapipa akitokea kazini, alipigwa risasi. Mimi nilikuwa China na nilipoambiwa nilipatwa na mshituko mkubwa, nilijaribu kuwasiliana naye ikashindikana.
“Niliambiwa baadaye kuwa mume wangu alikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hakufika kwani alifia njiani. Nilirudi nchini Oktoba 8, mwaka jana na tukachukua mwili na kwenda kumzika mkoani Singida.

No comments:

Post a Comment