Thursday, August 9, 2012

Mbunge aishukuru Serikali kurudisha muswada wa mafao

MBUNGE wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), jana aliipongeza Serikali kwa kurudisha bungeni Muswada wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii  baada ya yeye kuwasilisha hoja bungeni akitaka muswada huo  urudi bungeni.  Sambamba na pongezi hizo, nalo Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limeipongeza Serikali kwa uamuzi huo ili wabunge waweze kujadili kwa undani vipengele ambavyo vimekuwa vikipingwa na wananchi wa kada mbalimbali.
Jafo alitoa pongezi hizo alipozungumzia uamuzi wa Serikali kukubali kuurudisha tena bungeni muswada huo ili kufanya mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012.  Jafo  alilishukuru Bunge, Serikali na Watanzania kwa ujumla kutokana na jinsi walivyokubali hoja yake ya kutaka kurejeshwa fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya huduma za jamii.

Alisema kitendo cha Bunge kukubali uwasilishwe bungeni muswada wa dharura kisha Serikali ikakubali kurejesha fao hilo, ni cha kiungwana kwa sababu inaonekana ni kwa jinsi gani vyombo hivyo vinavyowajali Watanzania.

“Kwanza kabisa sikutarajia kama nitaungwa mkono kiasi hiki, lakini baada ya kuwasilisha hoja yangu binafsi bungeni kisha Serikali ikaikubali hoja hiyo, ni dalili nzuri na inawapa matumaini wafanyakazi na wanachama wa mifuko hiyo. “Pamoja na kwamba sasa muswada utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria ya mifuko hiyo, kuna haja Serikali ikaandaa mazingira ya kuwabana wamiliki wa migodi ili wawalipe wafanyakazi wao mishahara minono kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu.

 “Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya wafanyakazi hao wa migodini wanalipwa fedha kidogo sana kiasi kwamba haziendani na mazingira wanayofanyia kazi na pia wazawa wanalipwa fedha kidogo kuliko wageni jambo ambalo linafaa kufanyiwa marekebisho.

“Vilevile kuna haja pia ya kuangalia namna ya kudhibiti saa za kufanya kazi kwani nilipotembelea baadhi ya migodi hivi karibuni ili kupata maoni ya wafanyakazi juu ya hilo fao la kujitoa, niliambiwa baadhi yao wanafanya kazi kwa saa 12 badala ya saa 8, hili nalo ni tatizo kubwa,” alisema Jafo. Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kipengere cha kuzuia mafao ya kujitoa kilikuwa kikiwakandamiza wafanyakazi.

Mwanzoni mwa wiki hii, Jafo aliwasilisha bungeni hoja binafsi akitaka fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya huduma za kijamii lirejeshwe ingawa lilikuwa limeondolewa. Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Bunge lilimuunga mkono na juzi Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema Serikali imekubaliana na mbunge huyo na kwamba muswada wa kurekebisha sheria ya mifuko hiyo utawasilishwa katika Bunge lijalo.

No comments:

Post a Comment