Showing posts with label siasa. Show all posts
Showing posts with label siasa. Show all posts

Monday, August 13, 2012

CCM YAWASHUKIA CHADEMA...


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye.

*Yadai wana njama za kuuza nchi kwa mataifa tajiri
*Yawataka wataje mabilioni yanayopewa nje na mikataba yake.
*Yasema harambee zao ni changa la macho
*Yahofia tamaa ya mataifa makubwa kwa rasilimali za nchi masikini
DAR ES SALAAM, TANZANIA 
CCM imesema imesikitishwa na iliouita usanii mkubwa unaofanywa na  Chadema, kuwahadaa Watanzania kwa kufanya harambee kwa lengo la  kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yanayodaiwa kutolewa  na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye aliyasema hayo jana,  Agosti 12, 2012, wakati  akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijijni Dar es salaam.
“Itakumbukwa mara kadhaa Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii  kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa chama hicho wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi  siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012, kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni." alisema Nape.
Alisema ,umekuwa ni utamaduni wa Chadema kuhadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii kina wanapokuwa wameshapewa mabilioni ya fedha na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe kuwa fedha wanazotumia zimetokana na michango ya watanzania wakati si kweli.
Nape alisisitiza kuwa CCM wanao ushahidi  kuhusu zinakotoka fedha na mikataba wanayoingia Chadema na wafadhili hao na kudai kuwa kama hawatasema wenyewe basi yeye (Nape) ipo siku atawasaidia kwa kutaja wafadhili hao na kuanika hadarani mikataba hiyo.
“Tunao ushahidi wa kutosha unaoonyesha mabilioni waliyopewa Chadema juzi na wafadhili kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni zao mbalimbali nchini. Cha kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania kwa jumla mikataba na wanakoyapata mabilioni haya, wanawahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato hayo mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama”, Alisema Nape
Nape alidai kwamba, siri kubwa inayofichwa kuhusu mikataba na mabilioni wanayopewa Chadema ni kwa sababu wanaotoa fedha hizo wana ajenda  ya kunyemelea rasilimali za nchi hii zinazoanza kuonyesha matumaini ya kuwepo kwa wingi ili wapate kizikwapua kwa urahisi kupitia mgongo wa chama hicho.
"Kwanini mabilioni hayo yanatolewa kwa Chadema wakati huu ambapo sasa Tanzania imo katika kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? Na Je ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe?", Nape alihoji.
Alisema, hatua hiyo ya Chadema itaitumbukiza Tanzania katika machafuko yasiyoisha, kama ambavyo inashuhudiwa katika baadhi ya nchi zenye rasilimali kama madini ambako nchi zenye utajiri wa fedha zilijipenyeza kupitia walioitwa wapambanaji wa uhuru na haki katika nchi hizo na hadi sasa hakuna amani.
"Migogoro mingi tunayoshuhudia hasa katika nchi zinazoendelea pamoja na kuwepo sababu zingine lakini moja ya chanzo kikubwa ni uwepo wa utajiri wa rasilimali mbalimbali ambapo mataifa makubwa huzitamani na njia pekee ya kuzipata kwa urahisi ni kuchochea migogoro ya ndani na hivyo kuwa rahisi kupora rasilimali hizo  wakati wenye nchi wanahangaika katika migogoro na kuachwa wakiwa masikini wa kutupwa huku waadhirika wakubwa wa migogoro na vita hivi vikiwanufaisha wakubwa.” Alisema Nape.
Nape alitoa mwito kwa Watanzania kuwa ni muhimu macho na ulaghai huo wa Chadema na wafadhili wao na kukitaka chama hicho na wafadhili wao kama kweli wana nia njema na Tanzania, waweke wazi mashariti ya ufadhili huo wa mabilioni ya fedha ili Watanzania wote wajue kama yana manufaa kwao au la hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya siasa hapa nchini vinaendeshwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo Watanzania wana haki ya kujua.
Pamoja na kuwataka kuweka wazi mashariti yanayoambatana na mabilioni hayo Nape aliwataka Chadema waseme hadharani wenyewe kwamba wamepewa mabilioni hayo,  na  kuwataka waache mara moja kuwahadaa Watanzania na kujaribu kujipachika kuwa ni Chama cha wanyonge kinachotegemea kujiendesha kwa michango ya watanzania huku wakiendelea kuchukua mabilioni kwa siri kutoka nje.
“Wasipowaeleza watanzania ukweli , tutawasidia  kuwaeleza watanzania ukweli wa kiasi halisi cha mabilioni haya, walikozitoa na mikataba waliyoingia. Lengo la hili ni kuhakikisha kuwa nchi yetu haiwekwi rehani kwa uroho wa madaraka wa baadhi ya wana siasa.” Nape alisema.
Nape akawaasa wanasiasa, kuendesha  siasa za nchi kwa kuzingatia uzalendo na kukwepa kudumbukia kwenye tamaa za madaraka kujisahau na kuwa tayari hata kuweka nchi  rehani, hasa kipindi hichi ambapo ugunduzi wa rasilimali mbali mbali hasa madini, gesi na mafuta vikiwa vinashika kasi nchini na kwamba ugunduzi huo uwe baraka kwa nchi badala ya laana na kuwa chanzo cha kuiuza nchi.
CHANZO: www.ccmchama.blogspot.com


Mnyika Ajibu Mapigo Ya Nape...!



Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini.

Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo: Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu.

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali. CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko. Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.

Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.

Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.

Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani. Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.

CCM inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.

Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.

Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya kweli.CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.

CHADEMA tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM. CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.

CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi. Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.

Mikakati yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

12/08/2012- Dodoma

Sunday, August 12, 2012

Makubwa Ya Wiki Iliyopita: Lema Kaondoka London, Nyuma Kaacha Zogo!

Godbless alifika London kufungua tawi la Chadema. Zogo lilianza hata kabla ya tawi kufunguliwa. Kisa? Mkutano ulifanyikia Pub. Shughuli ilifanyika na Godbless akaondoka London. Nyuma akaacha zogo kubwa. Naam, Mwenyekiti mpya wa Chadema tawi la London, Chriss Lukosi akawa ameanza kazi na vita. Ndio,  Wafuasi wa pande zinazosigana kiitikadi wakaendelea kunyukana mtandaoni. Kuna mpaka aliyemsema mwenyekiti mpya wa Chadema London kuwa ni mtu anayevaa koti hilo hilo moja kila anapokwenda. Mzee wa  kauka nikuvae! Hakyamungu, siasa ni burudani pia.

LEMA AMWOMBA SLAA AGOMBEE ARUSHA MJINI






MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini, Godless Lema amesema anatamani Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa agombea ubunge wa jimbo hilo akieleza anaamini atatoa mchango mkubwa zaidi kwa chama kabla ya mwaka 2015.Lema alitoa kauli hiyo juzi usiku jijini Dar es Salaam, wakati wa harambee ya kuchangia chama hicho kwenye kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko maarufu kama Movement for Change (M4C) mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema katika chama hicho kuna watu wengi wanaoweza kuwa wabunge wa jimbo hilo, lakini yeye binafsi angependa Dk Slaa awe mbunge wa Arusha Mjini kwa sababu Katibu Mkuu huyo wa Chadema akiwa bungeni ni moto wa kuotea mbali.

Lema alisema: “Kuhusu ubunge wa Arusha sina hofu, atakuja Dk Slaa au mimi, ingawa sasa napenda aje Dk Slaa.”
Alisema angefurahi kama Dk Slaa angekuwa mbunge wa jimbo hilo hasa katika kipindi hiki cha kutafuta mabadiliko kumpokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Lema alisema hivi sasa anafurahia mchango mkubwa anaoutoa katika chama chake akiwa nje ya Bunge.
“ Nahisi kutoa mchango mkubwa katika chama nikiwa nje ya Bunge kuliko nilivyokuwa bungeni kwa sababu nimefanya shughuli nyingi zenye matokeo chanya katika taifa hili,” alisema Lema.

Lema alienguliwa ubunge mwaka huu na Mahakama ya Kuu Kanda ya Arusha kwa kilichoelezwa kuwa alitumia lugha chafu katika kampeni za kuusaka ubunge huo mwaka 2010.

Kuchangia fedha za M4C
Lema alieleza kuwa fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zitatumika kununulia helikopta, magari, pikipiki, baiskeli na matumizi mengine ya Chadema kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa ukombozi kwa wananchi.

“Tusifanye siasa ili kutafuta vyeo bali tulenge kuleta mabadiliko chanya katika jamii iliyonyanyasika kwa muda mrefu. Nchi yetu ilipata uhuru, lakini sasa tunahitaji mabadiliko yanayowakomboa wananchi kutoka kwenye umasikini,” alisema Lema.

Kauli ya Mbowe
Akizungumza katika harambee hiyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa, propaganda za ukabila, udini na rangi zinazoenezwa na CCM ni dhaifu na zimeshindwa kuidhoofisha Chadema.

Alisema kuwa wananchi wamezishtukia propaganda hizo na kwamba, wananchi wengi wamehamasika kutaka mabadiliko.
Katika harambee hiyo zaidi ya Sh270 milioni zilipatikana, kati ya hizo Sh250 milioni zikiwa ni ahadi na Sh20 milioni zikiwa ni fedha taslimu.
Kati ya fedha hizo, Sh20 milioni zilichangwa na tawi la Chadema nchini Marekani likiwa na majimbo yake Washington DC, Maryland na Virginia.

Watendaji wa Serikali
Kivutio kikubwa kilikuwa kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kuchangia katika harambee hiyo na kutaka waitwe Wasamaria wema bila kutaja majina yao.

Mbowe alisema: “Kwa kuwa wananchi wametuamini, tumeacha njia ya maandamano na sasa tunataka kufika kila kata ya nchi hii ili kufikisha ujumbe wa mabadiliko kwa wananchi. "

Alisema kuwa wamekubaliana baada ya kumalizika kwa kikao cha Bunge wabunge wote wa Chadema watasambaa nchi nzima kueneza Vuguvugu la Mabadiliko.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kuwa mbali ya kufika kwenye kila kata chama hicho pia kimejipanga kufikisha ujumbe huo katika nchi zote ambako kuna Watanzania.

“ Hatuna mchezo sasa, tumejipanga kuchukua dola ifikapo 2015, hawa CCM sasa ni kama wanaweweseka hawajui wanalolifanya, tutawang’oa tu, ” alisema Mbowe.

Alisema kuwa chama hicho kikifanikiwa kuchukua dola, kipaumbele kikubwa kitakuwa ni kuboresha elimu ambayo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya taifa.

“ Kipaumbele namba moja, mbili hadi tatu kitakuwa ni elimu. Tutawekeza zaidi kwenye elimu ili kuwawezesha wananchi kuhimili changamoto za dunia ya sasa hasa katika usimamizi wa rasilimali zao,” alisisitiza Mbowe.
Aliwahimiza watu wanaokichangia chama hicho kwa kuficha majina yao kuacha hofu akisema: “Jitokezeni hadharani, hamna sababu ya kuhofu kama kweli mnahitaji mabadiliko. Tumepuuzwa, tumenyanyaswa na tumedhalilishwa kiasi cha kutosha, sasa basi tuache woga.”

Alisema kuwa, CCM imeshindwa kuwasikiliza madaktari, walimu na wafanyakazi wengine lakini Chadema inaahidi kushughulikia matatizo ya makundi hayo.
Akizungumzia umuhimu wa harambee hiyo, Mbowe alisema mabadiliko yana gharama zake na kwamba wadau ndiyo wanapaswa kuchangia chama hicho.
Mbowe aliomba kila mpenda mabadiliko kuchangia kwa kadri ya uwezo wake na kwamba fedha zake zitailetea mabadiliko nchi hii.

Vyeo
Akizungumzia suala la nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, Mbowe alisema kuwa, huu si wakati wa kugawana vyeo wala kutangaza nafasi za kugombea bali kukiimarisha chama ili kiweze kuwa na nguvu zaidi.
Naye Mwenyekiti wa M4C, Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mayunga alisema harambee hiyo ilikuwa na lengo la kukusanya Sh5 bilioni katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema katika hafla ya jana walipanga kupata Sh500 milioni, lakini hazikutimia kutokana na msongamano wa wananchi waliokuwa wakituma fedha kwa njia ya simu za mkononi.

“Tunadhani hadi kesho (leo) kiasi hicho kitatimia kwa sababu wananchi wengi wametuma fedha lakini bado hazijatufikia,” alisema Mayunga.
Aliwataka wananchi kutuma fedha kwa kutumia njia ya simu za mkononi kwa sababu hiyo ndiyo njia rahisi. 

 







 

Thursday, August 9, 2012

Mbunge aishukuru Serikali kurudisha muswada wa mafao

MBUNGE wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), jana aliipongeza Serikali kwa kurudisha bungeni Muswada wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii  baada ya yeye kuwasilisha hoja bungeni akitaka muswada huo  urudi bungeni.  Sambamba na pongezi hizo, nalo Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limeipongeza Serikali kwa uamuzi huo ili wabunge waweze kujadili kwa undani vipengele ambavyo vimekuwa vikipingwa na wananchi wa kada mbalimbali.
Jafo alitoa pongezi hizo alipozungumzia uamuzi wa Serikali kukubali kuurudisha tena bungeni muswada huo ili kufanya mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012.  Jafo  alilishukuru Bunge, Serikali na Watanzania kwa ujumla kutokana na jinsi walivyokubali hoja yake ya kutaka kurejeshwa fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya huduma za jamii.

Alisema kitendo cha Bunge kukubali uwasilishwe bungeni muswada wa dharura kisha Serikali ikakubali kurejesha fao hilo, ni cha kiungwana kwa sababu inaonekana ni kwa jinsi gani vyombo hivyo vinavyowajali Watanzania.

“Kwanza kabisa sikutarajia kama nitaungwa mkono kiasi hiki, lakini baada ya kuwasilisha hoja yangu binafsi bungeni kisha Serikali ikaikubali hoja hiyo, ni dalili nzuri na inawapa matumaini wafanyakazi na wanachama wa mifuko hiyo. “Pamoja na kwamba sasa muswada utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria ya mifuko hiyo, kuna haja Serikali ikaandaa mazingira ya kuwabana wamiliki wa migodi ili wawalipe wafanyakazi wao mishahara minono kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu.

 “Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya wafanyakazi hao wa migodini wanalipwa fedha kidogo sana kiasi kwamba haziendani na mazingira wanayofanyia kazi na pia wazawa wanalipwa fedha kidogo kuliko wageni jambo ambalo linafaa kufanyiwa marekebisho.

“Vilevile kuna haja pia ya kuangalia namna ya kudhibiti saa za kufanya kazi kwani nilipotembelea baadhi ya migodi hivi karibuni ili kupata maoni ya wafanyakazi juu ya hilo fao la kujitoa, niliambiwa baadhi yao wanafanya kazi kwa saa 12 badala ya saa 8, hili nalo ni tatizo kubwa,” alisema Jafo. Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kipengere cha kuzuia mafao ya kujitoa kilikuwa kikiwakandamiza wafanyakazi.

Mwanzoni mwa wiki hii, Jafo aliwasilisha bungeni hoja binafsi akitaka fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya huduma za kijamii lirejeshwe ingawa lilikuwa limeondolewa. Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Bunge lilimuunga mkono na juzi Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema Serikali imekubaliana na mbunge huyo na kwamba muswada wa kurekebisha sheria ya mifuko hiyo utawasilishwa katika Bunge lijalo.

Mnyika ‘avalia njuga’ sheria za hifadhi ya jamii


Reginald Miruko
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika anakusudia leo kutangaza utaratibu wa kusanya saini za wabunge wasiopungua 10 ili kuunga mkono mpango wake wa kuwasilisha bungeni muswada binafsi wa marekebisho ya sheria za
hifadhi ya jamii ili kurejesha fao la kujitoa linalolalamikiwa nchini kote.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema uamuzi huo umetokana na ushauri wa wabunge wenzake na maoni ya wafanyakazi aliyoyakusanya kwa njia mbalimbali ikiwamo ya mtandao Agosti 4 na 5 mwaka huu.

“Nitaeleza utaratibu wa kukusanya saini za hati ya dharura ya muswada baada ya mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira na majumuisho ya waziri husika,” alisema Mnyika.

Agosti 3, mwaka huu mbunge huyo alieleza kuwa mgogoro uliopo chanzo chake, mbali na marekebisho ya sheria yaliyofanyika Aprili 13, ni
tafsiri potofu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuhusu marekebisho hayo, kuhusu fao la kujitoa.

Alisema tatizo kubwa halikuanzia katika marekebisho ya mwaka huu, bali ni udhaifu wa mfumo wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii ambao unahitaji marekebisho makubwa.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa muswada atakaowasilisha bungeni unahusu fao linalolalamikiwa na mambo mengine ambayo hakuyaweka wazi.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kufuta kifungu kinachoruhusu fao la kujitoa na kuzua malalamiko kwa wafanyakazi na wanaharakati nchi nzima, kuwa sheria hiyo imelenga kuwanyima haki.

Katika baadhi ya maeneo, hasa migodi imedaiwa kuwa baadhi ya wafanyakazi wameanza kugoma na wengine kuacha kazi baada ya kubaini kuwa hawataweza kupata fedha zao na mafao kabla ya kufikisha miaka 55 na kustaafu kwa hiyari au miaka 60 ya lazima.

Vigogo wachuana uchaguzi UVCCM, UWT

ZAIDI ya wagombea 83 wamechukua na kurudisha fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi zilizotangazwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wakiwamo watoto na jamaa wa vigogo. Wakati mnyukano ndani ya UVCCM ukishika kasi, mpambano mkali unaonekana pia kuwapo katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), baada ya wagombea tisa wakiwamo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Terezya Huvisa na Mbunge wa Viti Maalumu, Rita Mlaki kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti.

Vigogo wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba ambaye ndiye mwenyekiti wa umoja huo sasa na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela. Mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ulikamilika jana.  UVCCM Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Oganaizesheni na Siasa UVCCM, Sophia Duma alisema makada hao 83 waliochukua na kurudisha fomu hizo, wanawania nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti na umakamu mwenyekiti.

 Wakati nafasi ya mwenyekiti ikiombwa na watu tisa, 18 wanawania nafasi ya makamu mwenyekiti. Makada hao wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Afrika Mashariki Paul Makonda ambaye pia ni mshirika wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma Anthony Mavunde na Mboni Mhita ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Kondoa Kaskazini. Wengine ni Mwenyekiti wa UVCCM, Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wengine ni Abubakar Asenga na Sango Gungu, Augustino Matefu, Ali Salum, Adolf Florian, John Beya, Peter Lwena na Innocent Melesi. Pia wamo Faidha Salum, Masoud Khamis, Felician Mtewele, Daud Mtungu na Theresia Mtelele. Nafasi nyingine ni 33 ambazo ni za kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC). Nafasi ya ujumbe wa Nec imeombwa na makada 33 uwakilishi wazazi wajumbe wanne na makada 32 wameomba nafasi ya Baraza Kuu ya UVCCM Taifa.

UWT Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makiladi alisema kwamba waliorejesha fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti wa umoja huo ni tisa na nafasi ya makamu mwenyekiti watatu. Aliwataja wanaowania nafasi ya mwenyekiti kuwa ni Sofia Simba, Anne Kilango Malecela, Maryrose Magige, Terezya Huvisa, Hamida Hassan Thabit, Halima Mamuya, Hilda Omary Kitana, Rita Mlaki na Raya John Safari.

“Waliorejesha fomu za kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Asha Bakari Makame, Asha Abdallah Juma na Sheilla Anna Ahmed,” alisema Makiladi. Alisema nafasi nyingine zinazowaniwa ni za wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Baraza Kuu UWT Taifa, Mwakilishi UWT kwenda mkutano wa UVCCM na Mwakilishi wa UWT katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi. Nafasi nyingine ni zile za kila mkoa ambazo ni Mwenyekiti, Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa, wajumbe wawili kutoka kila wilaya.

“Pia wapo ambao wanawakilisha wilaya zao katika baraza la mikoa na nafasi mojamoja kutoka jumuiya ya wazazi,” alisema  Makiladi. Alisema idadi ya wagombea wote waliochukua fomu itatolewa leo na kuongeza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, wamejitokeza wagombea wengi zaidi.

Lissu aingia matatani

MNADHIMU wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ameshtakiwa kwenye Kamati ya Kinga, Haki na Maadili ya Bunge kutokana na kauli yake kuwa baadhi ya wabunge waliokuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini wana mgongano wa kimasilahi.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na mbunge aliyefungua malalamiko hayo, Charles Mwijage  (Muleba Kaskazini-CCM), zinasema kuwa mbunge huyo wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, alimkashifu.

Hivi karibuni, Tundu Lissu alizungumza na waandishi wa habari bungeni na kuwataja wabunge saba kuwa wana mgongano wa kimasilahi kwenye Kamati ya Nishati na Madini.

Wabunge hao wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Sara Msafiri (Viti Maalumu), Mariam Kisangi (Viti Maalumu), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Vicky Kamata (Viti Maalumu), Yusuph Nassir (Korogwe Mjini),  Charles6 Mwijage (Muleba Kaskazini) na Munde Tambwe (Viti Maalumu).

Akizungumza na Mwananchi juzi, Mwijage alikiri kumwandikia Spika wa Bunge, Anne Makinda kumlalamikia kuhusu Lissu.

 “Ni kweli nimemwandikia barua Spika na nimeshaikabidhi, nataka shauri letu lisikilizwe na nitendewe haki,” alisema.

Alisema kutokana na matamshi ya Lissu, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ilimwandika kuwa ni mla rushwa na kuathiri hadhi yake.

Mwijage pia amelilalamikia gazeti la Tanzania Daima kuwa liliandika habari hiyo kwa kumtaja kuwa ni mla rushwa na baadaye likasambazwa jimboni kwake kwa masilahi ya kisiasa.

Kwa upande wake, Lissu alisema hajaitwa na Kamati ya Bunge kuhusu suala hilo lakini alikiri kupata taarifa hizo kutoka kwa Mwijage.

“Nimekutana na Mwijage akaniambia amenishtaki na mimi nimemuuliza ‘unajua nilichokisema?’ na yeye akaniuliza kwani ulisema nini? Nimemweleza kuwa mimi nawajibika kwa maneno yangu kuwa yeye ana mgomgano wa kimasilahi kwa kuwa consultant (mshauri ) wa kampuni ya Puma. Siwezi kumwita mtu mla rushwa kwa kuwa sina ushahidi na hilo,” alisema na kuongeza: