Wednesday, August 15, 2012

Wasiolipa Ada Kutofanya Mitihani Ya Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA)

Kiongozi wa Serekali ya Wanafunzi akimuunesha orodha ya Wanafunzi ambao majina yao yanasubiri malipo yao kutoka Bodi ya Mkopo ya Elimu ya Juu .

Na Mwanajuma Mmanga
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimezuwiya kufanya mitihani kwa wanafunzi wote ambao hawajakamilisha ada za masomo hali ambayo imepelekea mgongano na mizozo baina ya wanafunzi na uongozi wa chuo hicho.

Kauli hiyo imetolewa na wanafunzi wa chuo hicho walipokuwa katika maandamano ya kudai haki yao kufanya mitihani hiyo.

Mmoja miongoni mwa wanafunzi wa chuo hicho Ali Kombo alisema wiki moja baadae tunatarajia kufanya mitihani hiyo ghafla wanapokea taarifa ya kuwa kila mwanafunzi hajakamilisha malipo ya ada hatomruhusu kufanya mtihani jambo ambalo ni kinyume na matakwa yao.

Pia alisema kuna baadhi ya wanafunzi wanalipiwa na bodi ya mikopo la taifa lakini mpaka sasa hawajaingiziwa fedha hizo hali ambayo inarejesha nyuma masomo yao.

"Sisi baadhi yetu tushalipiwa na bodi kwa asilimia 90 na kumebaki asilimia 10 tu kwanini wakatuzuilia kutofanya mitihani hiyo. hii fedha kama asilimia 80 ishalipiwa na bodi wakati hela hiyo inakuja moja kwa moja inaingia kwenye akaunti" alisema.

Kwa upande wa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho Ali Sharifu Kombo, alisema kuwa yeye binafsi kwa kushirikiana na uongozi wa serikali yake wameshafuatilia kwenye bodi ya mikopo Tanzania na kuhakikishiwa kuwa fedha hizo tayari wameshaingiziwa.

Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Idrisa Rai alisema fedha za wanafunzi hao bado hazijaingizwa nao kama uongozi wanalalamikia kudai ada za masomo ya wanafunzi kwa lengo la maendeleo ya chuoni hapo.

Sambamba na hilo Nae Kaimu Meneja wa Bodi ya Mikopo Tanzania, Patric Show alisema fedha za wanafunzi hao tayari zimeshaingiziwa katika akaunti zao na hivyo inawezekana ikawa ni kuchelewa kwa mawasiliano baina ya bodi na Uongozi wa chuo hicho.

Meneja huyo wa bodi hiyo alisema mchakato mzima uliosababisha kuchelewa kwa kufika barua hiyo katika bodi ya mikopo Dar es Salaam kwa muhusika mkuu ni Sajent wa bodi, lakini kumbe kabla ya hapo Mhasibu wa chuo hicho, Rukia tayari ameshaingiziwa tokea jana.

Kutokana na kuchelewa kwa kupelekwa kwa barua hiyo tayari zimeshaingizwa ndani ya akaunti zao kwa kila mwanafunzi ambae yuko chuoni hapo.

Meneja huyo amekiri kuwa fedha hizo tayari zimeshaingizwa ndani ya akaunti hizo jumla ya shilingi milioni 13, kwa orodha ya wanafunzi 58 wa chuo SUZA.

Hivyo amewataka wanafunzi hao kuwa wastahamilivu katika kuvuta subra na kuwa wasikivu kwani mipango yote ishakaa sawa na kila mmoja atapata haki yake na atafanya mtihani huo.

No comments:

Post a Comment